NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia
Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila ameagiza wakandarasi wanaojenga barabara
za Engosheraton, Olasiti na Oljoro patakapojengwa stendi mpya ya mabasi kwa
Jiji la Arusha zikamilike kwa wakati.
Agizo hilo lilitolewa Jijini hapa na Mhandisi Mativila
wakati alipotembelea barabara hizo tatu zenye urefu wa kilomita 12.1 kupitia
Mradi wa Kuboresha Miji (TACTIC) uliopo
chini ya TARURA.
Alisema barabara hizo tatu za Engosheraton, Olasiti na
Oljoro zenye thamani ya shilingi bilioni 15.4 zinajengwa kwa kiwango cha lami
lakini bado ukamilishwaji wake upo nje ya muda.
Akizungumza mara baada ya kutembelea barabara hizo Mhandisi
Mativila alisema ziara hiyo ni ya kawaida katika kuangalia maendeleo ya kazi
zinazofanywa katika ujenzi wa barabara hizo.
“Ujenzi wa barabara ya Oljoro bado upo nyuma kwa asilimia 35
kutokana na kubadilishwa kwa mchoro(dizaini) kutokana na kiwango chake cha
usanifu na kuwa barabara ya Mkoa kutokana na ujenzi wa stendi mpya ya mabasi.”
“lakini pia barabara hii itakuwa ni kiunganishi cha barabara
kuu inayoenda hadi Dodoma hapo baadaye,” aliongeza Mhandisi Mativila.
Hata hivyo alisema tathimini ya kuongeza muda wa ujenzi wa
barabara hiyo ya Oljoro imeshafanyika kwasababu mradi huo ulipaswa kukamilika
mwishoni mwa mwezi huu.
"Tulipaswa kuwa asilimia 99 katika mradi huu na sasa
wakandarasi wanatakiwa kukamilisha mradi huo Juni mwaka huu huku mvua
zikitegemea kunyesha muda wowote hivyo lazima wakamilishe barabara hizi."
Pia alisisitiza mradi huo wa barabara hizo tatu kukamilika
kwa haraka ili Juni mwaka huu, zikabidhiwe na kusisitiza ubora ni jambo la
msingi sana.
"Sijaridhika na hatua hii lakini kuna changamoto
zilijitokeza hivyo wazirekebishe kwani serikali inatumia fedha nyingi katika shughuli
za maendeleo hivyo lazima wasimamizi na wajenzi wa barabara hizi wakamilishe
kwa wakati.”
Naye, Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya ujenzi ya
Mhandisi Consultant Ltd, Mhandisi John Benedict alisema kama wahandisi
wnashukuru kwa serikali kukubali changamoto hizo huku akiahidi kwamba
mradi huo utakamilika Juni mwaka huu.
Aidha, alisema wataongeza timu ya kazi ili kupima maendeleo
ya mradi anaojenga mkandarasi huyo ili kufikia malengo kwani mradi huo
unatembelewa mara kwa mara huku mkandarasi analipwa kwa wakati.
Awali Mhandisi Sofa Edward kutoka Jiji la Arusha ambao wao ndio wasimamizi wakuu aliahidi kusimamia wakandarasi hao ili wamalize kwa wakati kazi hiyo kwani wananchi wa kata hizo wanazihitaji kwaajili ya kurahisisha usafiri ikiwemo wananchi kupata maendeleo.
0 Maoni