Imeelezwa lengo la Serikali la kuanzisha Vituo vya Mfano kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uchimbaji bora kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini limefaniliwa kwa kiasi kikubwa baada ya wachimbaji wengi nchini kuhamia na kuanzisha teknolojia ya Uchenjuaji wa kutumia (CIP) badala ya mialo ambayo imesaidia kuongeza tija kwenye shughuli zao na kuondokana na uharibifu wa mazingira.
Hayo
yamebanishwa na Mshauri Elekezi katika shughuli za uchimbaji mdogo, Mkurugenzi
wa Kampuni ya Tan Discovery Consultant Company Limited na mjenzi wa vituo
hivyo, Mhandisi Rogers Sezinga wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini baada ya kuvitembelea vituo
hivyo.
Ameongeza
kwamba, vituo vya mfano vimesaidia kuongeza mzunguko wa uuzaji madini kwenye
masoko jambo ambalo limepelekea Serikali kupata taarifa za wachimbaji hao na
hivyo kuwawezesha kupata mikopo kwenye baadhi ya taasisi za fedha hapa nchini.
‘’ Nikiwa
mshauri elekezi, nimekuwa nikipata maombi mengi kwa ajili ya ujenzi wa CIP hizi
kutoka maeneo mbalimbali nchini. Hadi sasa nimejenga CIP zaidi ya 10 na hapa
kama mnavyoniona naendelea na ujenzi wa CIP nyingine, hivyo vituo hivi
vimeongeza tija baada ya watu kujifunza. Wito wangu, wachimbaji wazitumie ili
kuachana na matumizi ya zebaki na zitaongeza vipato vyao na kodi za Serikali,’’
amesema Sezinga.
Mbali na
kuanzishwa CIP, vituo hivyo vimewavuta
wakazi wanaozunguka vituo hivyo na
wachimbaji kujikita kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya
dhahabu baada ya kutoa elimu kwa vitendo kuhusu namna bora ya uchimbaji na
uchenjuaji wa madini kwa wachimbaji wadogo.
Vituo vya
mfano vilijengwa na Serikali kupitia Wizara ya Madini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo
kilichopo kijiji cha Katente Wilayani Bukombe, Lwamgasa- Geita na
Itumbi-Chunya, vinasimamiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) likisimama
kama mlezi wa wachimbaji wadogo.
Aidha, mbali
na mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji, vituo hivyo vinatoa huduma za uuzaji wa
vilipuzi, kemikali, uchomaji wa kaboni ambapo mpaka sasa Vituo hivyo
vimekusanya zaidi ya bilioni 3.3 zikitokana na kodi mbalimbali na mrabaha tangu kuanzishwa kwake Mwaka wa Fedha
2019- 2020.
Kwa upande
wake, Msimamizi wa Kituo cha Mfano cha
Katente ambaye pia ni Mratibu wa Vituo vya Mfano vya Katente-Bukombe, Lwamgasa-Geita na Itumbi-Chunya, Mhandisi
Tiberio Lucian Kaduma amesema Serikali kupitia STAMICO imejenga Vituo hivyo
katika maeneo yenye madini kwa lengo la kumsaidia mchimbaji mdogo kupata
maarifa ya uchimbaji na uchenjuaji bora na wenye tija.
Aidha,
Mhandisi Kaduma amesema Vituo vya Mfano ni sehemu mahususi ya kuwapatia
wachimbaji wadogo mafunzo ya nadhari na vitendo ili kukuza ujuzi, maarifa na
elimu kuhusu uchimbaji salama na utunzaji wa mazingira.
Mhandisi
Kaduma amesema Vituo hivyo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa kuhusu
uchimbaji salama ikiwemo uchenjuaji wa kutumia teknolojia ya sayanaidi katika
uchenjuaji na kuachana na matumizi ya zebaki inayo haribu mazingira.
‘’Serikali
kupitia STAMICO inampango wa kujenga vituo vya mfano vingine katika mikoa ya
Kimadini ya Tanga Lindi na Kahama ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya
shughuli za uzalishaji madini kwa faida na kuongeza tija kwenye Pato la Taifa.
Pamoja na mambo
mengine, Mhandisi Kaduma ametoa wito kwa wachimbaji madini kote nchini
kuvitumia Vituo vya Mfano kwa ajili ya maendeleo yao na kutumia huduma
zinazotolewa na Vituo hivyo ikiwemo uuzaji wa vilipuzi na kemikali zinazotumika
katika uchenjuaji madini ili kujiongezea wigo na ufanisi katika shughuli za
uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini.
Kwa upande
wake, mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu wa Katente namba 1, Max Thomas
Kajoro ambaye ni mnufaika wa kituo hicho, ameishukuru Serikali kupitia STAMICO
kwa kujenga Kituo cha Mfano cha Katente ambacho kimemnufaisha kwa kiwango
kikubwa baada ya kupeleka mawe yake kwa ajili ya kuchakata na kupata dhahabu nyingi
zaidi ya matarajio yake ambapo ametoa wito kwa wachimbaji wengine kutumia Kituo
hicho kwa ajili ya maendeleo yao.
‘’Kituo cha
mfano Katente ni suluhisho na msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo ambapo mimi
binafsi kimenisaidia kununua mashamba, gari, pikipiki, kujenga nyumba,
kusomesha watoto na kukidhi kuhudumia familia yangu,’’ amesema Kajoro.
Naye, Mchimbaji
mdogo wa madini ya dhahabu wa Katente namba 2, Simon Sospeter Dittu ameipongeza
Serikali kwa kujenga Kituo hicho katika eneo hilo ambapo amenufaika kwa kupata
elimu ya uchimbaji salama na ushauri wa uchimbaji bora ikiwemo kutunza
mazingira na elimu ya utambuzi wa maeneo yenye tija katika uchimbaji wa madini
ambapo kwa sasa anazalisha kwa faida kupitia mgodi wake.
Kwa upande
wake, Mchimbaji mdogo Pamela James amelipongeza Shirika la STAMICO kwa kuwalea
vyema na kuwapa mafunzo ya uchimbaji na
uchenjuaji kwa vitendo jambo ambalo
limewasaidia wachimbaji wengi kuachana na mila potofu za kutumia waganga
na badala yake kutumia utaalamu waliyopatiwa na kujipatia faida ambapo kwa sasa
mama huyo ameajiri zaidi ya wafanyakazi 50 katika shughuli zake za uchimbaji.
Aidha, Pamela
ametoa wito kwa STAMICO kupanua wigo wa uzalishaji kwa kufunga mitambo mikubwa
zaidi ili kupunguza foleni ya wateja, muda na kuongeza uzalishaji tofauti ya
ilivyo sasa.
0 Maoni