Naibu Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amemtaka Mkandarasi M/s
Jiangxi GEO Engineering Group anayejenga barabara ya Kihonda - VETA yenye urefu
wa Km 12.85 kwa kiwango cha lami Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro kufanya
kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa ubora
unaotakiwa ndani ya miezi mitatu hadi kufikia mwezi Mei 2025.
Mhandisi
Mativila ametoa agizo hilo kwa mkandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri wa mradi
huo katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo unaotekelezwa kupitia Mradi wa
Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC) chini ya mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
“Nimekuja kutembelea moja ya miradi mikubwa
ambayo serikali ya awamu ya sita inatekeleza kwa ajili ya kuleta maendeleo na
ushindani katika miji 45 ya Tanzania iliyochanguliwa iwe na ushindani wa kuwa
na miundombinu bora ikiwemo ya barabara kwa kiwango cha lami inayowezesha kukua
kwa uchumi,’’ alisema.
Alisema kati
ya miji hiyo ni pamoja na Manispaa ya Morogoro ambayo inanufaika na utekelezaji
wa mradi huo mkubwa ambapo kwa mkoa huo mradi unagharimu kiasi cha shilingi
bilioni 19.6.
“Mradi huu
umechelewa na upo nyuma kwa asilimia 18 na kwamba umetekelezwa kwa asilimia 82
tu na kuna sababu kadhaa ambazo zimeelezwa, baada ya kuweka mambo sawa tunataka
mradi huu ukamilike ndani ya muda wa miezi mitatu endapo kukiwa na mvua kubwa
basi mradi uwe umekamilika Mwezi Augosti mwaka huu,” alisema.
Naye, Meneja
wa TARURA Wilaya ya Morogoro, Mhandisi Mohamed Muanda alisema ujenzi wa mradi
huo ulianza Oktoba 23, 2024 na kutakiwa kukamilika Februari 2025 ambapo awamu
ya kwanza inahusisha ujenzi wa mifereji mikubwa ya maji ya mvua kuelekea mto
Kikundi yenye urefu wa jumla ya Km 4.4, ujenzi wa ofisi ya Mhandisi Mshauri na
ofisi ya wasimamizi wa miradi.
Kwa upande
wake, Mwakilishi wa Mhandisi Mshauri kutoka nchini pamoja na Mhandisi Mshauri
kutoka Ethiopia (JV Core consultancy), Mhandisi Dargie Dilbedi alimhakikishia
Naibu Katibu kwamba kazi hiyo ipo katika hatua ya mwisho na kwamba anatumaini
ndani ya miezi mitatu ya nyongeza itakamilika.
0 Maoni