WANANCHI wa kijiji cha Liweta Halmashauri ya wilaya
Songea mkoani Ruvuma, wameishukuru Serikali kupitia Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuwajengea daraja la kudumu katika mto Liweta linalounganisha
kijiji hicho na Masuku na maeneo yao ya kilimo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema, awali walikuwa
wakipata shida kubwa kupitia katika eneo hilo hasa wakati wa masika wanapotaka
kwenda mashambani na vijiji vya jirani kutokana na kukosekana kwa kivuko hali
iliyochangia kuwarudisha nyuma kiuchumi.
Micheal William amesema,kabla ya daraja hilo walitumia
siku tatu hadi nne kusubiri maji yapungue ndipo waendelee na safari kwenda
kitongoji cha Litapatile na kijiji cha Masuku,lakini sasa hakuna tena
changamoto hiyo baada ya kujengewa
daraja la kudumu.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia kwa
kuboresha barabara hiyo hadi maeneo ya Litapatile ambako kuna uzalishaji mkubwa
wa mazao ya chakula na biashara ili wakulima waweze kuwa na uhakika wa
kusafirisha mazao yao.
“Wapo ndugu zetu waliofariki dunia kwa kusombwa na maji
walipokuwa wakijaribu kuvuka kipindi cha mvua kutokana na kukosekana kwa
daraja, lakini sasa baada ya kujengwa kwa daraja hili ni furaha na neema kubwa
kwetu”alisema.
Aidha, amesema, awali hali ilikuwa mbaya zaidi kwa watoto
wanaoishi mashambani kwani mto huo unapojaa maji walikaa muda mrefu kusubiri
hadi maji yapungue ili waweze kwenda shule hivyo kukosa baadhi ya vipindi
vya masomo.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Masuku Malaika Komba
amesema, miaka ya nyuma walikuwa kwenye mateso makubwa kupita katika eneo hilo
kutokana na kujaa maji mengi na pindi walipotaka kwenda upande mwingine
walitumia muda mrefu.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuangalia kwa jicho la
huruma na kutujengea daraja katika eneo hilo, hapa tumepoteza mazao yetu kwa
kusombwa na maji pindi tulipotaka kuvuka kwenda kijijini kutafuta masoko,”alisema
Komba.
Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Mhandisi Godfrey
Mngale amesema, Serikali imetumia Sh.milioni 449 kujenga daraja na kufanya
upanuzi wa barabara hiyo ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa
mazao kutoka shambani kwenda sokoni.
Amesema kuwa, daraja hilo ni muhimu katika kurahisisha
mawasiliano na itarahisisha kufungua maendeleo ya wananchi wa kijiji cha
Liweta, Masuku na Halmashauri ya wilaya Songea ambao walikuwa na uhitaji mkubwa
wa daraja la kudumu.
Mngale, ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya
daraja kwa kutojihusisha na vitendo vya kuchimba mchanga chini ya daraja, kuiba
alama za barabarani na kuacha kupitisha mifugo juu ya daraja kwani Serikali
imetumia gharama kubwa kujenga daraja na barabara.
Kwa upande wake meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma Mhandisi
Silvester Chinengo amesema, daraja la Liweta ni moja ya miradi ya kuondoa
vikwazo vya usafirishaji katika mkoa wa Ruvuma na daraja lina upana wa mita 20
na njia nne za kupitisha maji.
Mhandisi Chinengo amesema, daraja la Liweta linaunganisha
kijiji cha Liweta na Masuku na kabla ya kujengwa wananchi walikuwa wanapata
adha kubwa kupita kwenye maji na msimu wa kilimo walishindwa kwenda upande wa
pili kwaajili ya kuendelea na shughuli zao za uzalishaji.
“Kwa hiyo Serikali kupitia mradi wa kuondoa vikwazo vya
usafirishaji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ndiyo uliofanikisha ujenzi wa
daraja hili na kwa sasa wananchi wanafurahia huduma inayotolewa na Serikali yao
ya awamu ya sita,” alisema Chinengo.
Chinengo, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha
zilizotumika kujenga daraja hilo ambalo limewezesha kuondoa kikwazo cha
usafirishaji kilichowatesa wananchi wa maeneo
hayo kwa muda mrefu.



0 Maoni