Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Mogadishu, Shirikisho
la Jamhuri ya Somalia kwa ziara ya kikazi atakayoifanya nchini humo kuanzia
terehe 18 hadi 20 Disemba 2024.
Akiwasili nchini humo jana tarehe 18 Disemba 2024,
kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu, Waziri
Kombo amepokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo Nje Mhe. Balozi Ahmed Moalim
Fiqi na viongozi wengine waandamizi wa ngazi mbalimbali Serikalini.
Waziri Kombo akiwa nchini humo anatarajiwa kuongoza
ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Shirikisho la Jamhuri ya Somali yatakayofanyika jijini Mogandishu tarehe 19
Disemba 2024.
Mazungumzo hayo ambayo yataambatana na hafla ya kusaini
hati kadhaa za makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, vilevile
yanalenga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano, kukuza na kuimarisha ushirikiano
wa kidiplomasia na kiuchumi.
Aidha, mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua na kuongeza
fursa mpya za uchumi na biashara kwa manufaa ya pande zote mbili, ikiwemo
upatikanaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo mbili kama vile
mazao ya kilimo, bidhaa za viwandani na huduma mbalimbali ikiwemo usafiri wa
anga, afya na elimu.
Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo hayo utajumuisha
Watendaji na Viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel,
Viongozi waandamizi wa Vyombo vya ulinzi na Usalama na Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa.

0 Maoni