Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Benki ya CRDB wameendelea kutoa
elimu kuhusu Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara za Wilaya (Samia
Infrastructure Bond) kwa wadau mbalimbali mkoani Mwanza.
Elimu hiyo
imetolewa leo tarehe 06 Desemba, 2024 katika ukumbi wa Rock City Mall mkoani
Mwanza.
Akitoa
salamu za TARURA, Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Makori Kisare
amesema wao kama wasimamizi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara
za wilaya wamefurahi sana kwa kuanzishwa kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara (Samia Infrastructure Bond) iliyozinduliwa
rasmi na kwa mafanikio makubwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt Philip Mpango tarehe
29/11/2024 jijijini Dar es Salaam.
"Sisi
kama wanufaika wakubwa tumefurahi sana kwa kuanzishwa kwa hatifungani hii itakuwa ni miongoni mwa suluhisho kwa
wakandarasi wetu hasa wazawa kupata fedha za kutosha ambazo zitawawezesha
kutekeleza miradi kwa ufanisi na kulipwa kwa wakati kulingana na mikataba."
Amesema wazo
la kuanzishwa kwa hatifungani hii lilitoka kwa Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI,
Mhe. Mohamed Mchengerwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu
Hassan katika kutafuta njia sahihi ya kugharamia miundombinu inayosimamiwa na
TARURA.
"Kipekee
napenda kumpongeza na kumshukuru sana Mhe. Rais kwa maagizo yake ambayo Mhe.
Waziri aliyasimamia na sisi TARURA tumeyatekeleza," amesema.
Aidha,
Mhandisi Makori amewaomba wawekezaji mbalimbali ambao sio wakandarasi walio tayari kuwekeza katika hatifungani hiyo wasisite kuuliza maswali ili waweze kuelewa
zaidi kuhusu hatifungani hiyo ili wanapowekeza wajihakikishie wanawekeza sehemu
salama ambapo pia amewahakikishia kwamba hatifungani hiyo ni sehemu salama ya
kuwekeza.
Hatifungani
ya Miundombinu ya Barabara za Wilaya (Samia Infrastructure Bond) ni fursa nzuri
ya uwekezaji kwa Watanzania ambapo moja ya faida zitokanazo na uwekezaji wake
ni riba ya asilimia 12 kwa kila mwaka kwa miaka mitano.
0 Maoni