Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero mkoa wa Morogoro kuandika andiko maalum la mradi wa ujenzi wa standi ya mabasi Manyinga ili kuondoa adha ya miundombinu wanayokutana nayo wananchi katika kipindi cha mvua.
Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo baada ya kutembelea
stendi hiyo na kukuta hali isiyoridhisha huku Halmashauri ikiendelea kutoza
mapato katika standi hiyo.
“Mkiacha utaratibu ambao huwa mnaufanya wa kutenga mapato
ya ndani ambayo mnatenga bajeti kwaajili ya kufanya maendelezo madogo madogo
kuna utaratibu mwingine mnaweza kuutumia ambao ni kuandika andiko la mradi
kwasababu stendi hii inaonekana inaweza kuwa mradi wa kuzalisha mapato mengi
zaidi kwa ajili ya Halmashauri kwa sababu ya shughuli nyingi za kiuchumi
zinazofanyika,” amesema Mhe. Katimba.
Katika hatua nyingine, Mhe. Katimba amewaahidi wananchi
wa Mvomero kuwa serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Manyinga-Madizini
yenye urefu wa kilomita 3.9 ambapo serikali itatenga fedha taktibani bilioni
sita kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Jonas Van
Zeeland ameiomba serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuharakisha ujenzi
wa barabara hiyo ambayo ni hitaji la muhimu la kiuchumi kwa wakazi wa Mvomero.



0 Maoni