Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka Watanzania kujenga misingi ya kusaidiana kuheshimiana na
kuvumiliana ili kufanikisha malengo wanayojiwekea kimaendeleo.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo leo Desemba 15, 2024 Jijini
Dar es Salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni maalum katika Hafla ya Kutabaruku Jengo la
Kanisa la Waasventista Wasabato, Magomeni.
Amewahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuboresha
huduma za jamii na kuwekeza katika mipango itakayowezesha kukidhi mahitaji na
kupata Taifa endelevu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan siku zote amekuwa akisisitiza maridhiano, uhimilivu, mabadiliko
na kuimarisha amani yetu ili jamii iweze kupata maendeleo na kustawi,” amesema
Dkt. Biteko.
Aidha, amewataka waumini kuendeleza moyo wa kujitolea kwa
ajili ya uwekezaji na ujenzi wa miundombinu ya maendeleo kama vile kanisa na
miradi mingine ya kijamii.
Amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake
kuhakikisha kwamba misingi ya malezi na ushirikiano inayowekwa inafanikiwa.
“Wametajwa baadhi ya watu waliofanikisha ujenzi wa kanisa
hili la Magomeni, lakini pia wapo ambao hawakutajwa kwa kuwa hawakuwa tayari
kutajwa na hii ndiyo sababu kwao kutotajwa, sasa tuanze upya kila mmoja
ajitahidi kufanya jambo la kheri kwa mwenzie badala ya kumuumiza,” ameongeza
kuwa tuwe baraka kwa watu wengine na sio Kitunguu cha kuwatoa watu machozi
machoni,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mch. Dkt. Joel Okindo, Msaidizi wa
Mwenyekiti wa Divesheni ya Mashariki na Kati amewaka waumini kujenga moyo wa
kujitolea katika masuala ya maendeleo ili kutimiza azima ya uumbaji.
Amesema ujenzi wa Kanisa la SDA - Magomeni ulianza
takribani miaka 12 iliyopita na ujenzi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90
kutokana na michango ya waumini, wafadhili na viongozi mbalimbali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila
ametumia jukwaa hilo kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya mtu mmoja anayedaiwa
kutekwa ambapo amesema mtu huyo alitumia mbinu hizo baada ya kuuza gari
alilokuwa ameazima.
“Mhe. Naibu Waziri Mkuu, Dar es Salaam ni salama na huyu
mtu anayedaiwa kutekwa ni kwamba “amejiteka” baada ya kuazima gari na kuliuza,
Gari tayari tunalo na huyo mtuhumiwa atatokea hadharani hivi karibuni kuelezea
kilichotokea,” amesema Chalamila.
0 Maoni