Wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wamekaribishwa
kuwekeza mkoani Kagera kufuatia hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi
ambazo mkoa wa huo umefikia ikiwa ni pamoja na mipango ya maendeleo na fursa
nyingi za uwekezaji zilizopo.
Mkoa wa Kagera ni wa pili kwa uzalishaji wa samaki na
fursa ya uvuvi nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Mwanza fursa ambayo inawanufaisha
wakazi wake kwa kuwapatia ajira, lishe bora, kipato na maendeleo ya kiuchumi
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makazi bora kutokana na shughuli za uvuvi.
Akizungumza jana katika Uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba
mkoani Kagera wakati aliposhiriki katika Tamasha la Pili la Uwekezaji la mkoa
huo ikiwa sehemu ya Wiki ya Tamasha la Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani), Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa
wananchi wa mkoa huo kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani
mazao ya uvuvi, viwanda vya kutengeneza zana za uvuvi kama nyavu, kamba, vifaa
vya kujiokolea na mashine za boti badala ya kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya
nchi.
Dkt. Biteko amesema kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kitaifa
kuwa na ranchi 6 za mifugo kati ya ranchi 15 zilizopo nchini. Ametaja ranchi
hizo kuwa ni Missenyi, Mabale, Kikulula, Mwisa II, Kitengule na Kagoma.
Ameendelea kusema kuwa mkoa huo kupitia halmashauri zake
zote umetenga jumla ya hekta 345,430.97 kwa ajili ya malisho ya mifugo ambapo
uwepo wa maeneo hayo ya malisho na ufugaji yanatoa fursa kubwa ya uwekezaji kwa
kuanzisha ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa ili kuvutia
uanzishwaji wa viwanda vya kuchataka nyama na maziwa hasa katika maeneo yenye
ranchi za Taifa.
“ Naiona Kagera inakwenda kukua kwa kasi kubwa sana na
nitumie fursa hii kuwaomba na kuwaalika wawekezaji kote nchini na nje ya nchi
kuja kuwekeza Kagera kutokana na fursa zilizopo kwani mazingira ya uwekezaji ni
mazuri na uongozi wa mkoa umejipanga vyema kuwapokea na kuwahudumia kwa
viwango,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Kagera pia unaongoza kwa
uzalishaji wa zao la ndizi kwa wastani wa tani milioni 2.4 kati ya tani milioni
3.6 zinazozalishwa sawa na asilimia 60
ya uzalishaji wa zao hilo nchini. Kwa wastani zao la ndizi mkoani humo
linawaingizia wakulima kati ya shilingi bilioni 240 – 300 kwa mwaka, hivyo kuwa
na mchango mkubwa katika uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Pia, Dkt. Biteko amesema bado ipo fursa ya kuwekeza
kwenye teknolojia na miundombinu ya uchakataji wa zao la ndizi ili kuongeza
thamani na kuzalisha bidhaa nyingine zinazotokana na zao la hilo.
“Ninafahamu kwamba, mkoa umebuni na kuanzisha mradi wa
Mashamba Makubwa ya Kahawa yenye ukubwa wa ekari 10,000. Mradi ambao unalenga
kuwanufaisha watu wapatao 10,000 wakiwemo vijana na utatekelezwa kwa kipindi
cha miaka mitatu kuanzia 2024 – 2027. Kwa kuanzia tayari shamba lenye ukubwa wa
ekari 400 katika Kijiji cha Makongora wilayani Muleba ambapo kila kijana
amegawiwa ekari moja ya shamba lililoandaliwa na kupewa miche bure,” amesema
Dkt. Biteko.
Aidha, lengo la mradi huo likitajwa kuwa ni kuongeza
ajira kwa vijana, pato la mtu mmoja na pato la mkoa pamoja na kuongeza pato la
halmashauri kupitia ushuru wa zao la kahawa na kuliingizia Taifa fedha.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amesema kuwa
Tamasha la Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani), limelenga kuwakutanisha pamoja
wakazi wa Kagera na kuibua fursa za uwekezaji mkoani humo.
Amesema kuwa kupitia tamasha hilo wanautangaza Mkoa wa
Kagera licha ya kutokuwepo kwa jitihada za kufanya hivyo hapo awali ili
wananchi wa mkoa huo kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kuvutiwa na
fursa zilizopo na kwenda kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Tamasha la Ijuka Omuka 2024 limeanza Desemba 18, 2024 na
linatarajiwa kuhitimishwa Desemba 21, 2024. Tamasha hilo limesheheni matukio
mbalimbali ikiwemo maombezi kwa Mkoa wa
Kagera na Taifa, Kongamano la Uwekezaji,
maonesho ya biashara, tamasha la utamaduni, maonesho ya mavazi ya asili,
mashindano ya pikipiki na mechi kabambe ya mpira wa miguu Desemba 21, 2024 kati
ya Klabu ya Simba na Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba mkoani humo.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni