Wanawake wamuunga mkono Rais Samia Sekta ya Utalii

 

Wanawake zaidi ya 30 kutoka mikoa mitatu ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam wameamua kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza vivutio vya utalii nchini baada ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa nne kupanda mlima Sanje kutembelea Maporomoko ya maji Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa.

Zoezi hilo lilifanyika jana lilimhusisha pia mama mwenye mtoto wa umri wa miezi sita Agnes Samweli, ambapo baada ya kufika kwenye maporomoko alisema amekuwa akisikia kwa muda mrefu Hifadhi hiyo hivyo alipopata fursa aliamua kuja na mwanae kuitembelea.

Agnes alisema kuwa alipomsikia Rais Samia akitangaza vitutio vya utalii vilivyopo hapa nchini alihamasika kwenda kutalii na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa kuona maajabu ya Mungu ya maporokoko ya maji.

“Wakati mama Samia anatangaza vivuto vilivyopo nchini nilikuwa mjamzito na baada ya kujifungua mwanangu wa kike akiwa na miezi sita nimepata fursa ya kuja sikutaka kuiachia na ndiyo sababu nimekuja na mwanangu kutalii hapa Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa ili kutembelea maporomoko ya maji,” alisema Agnes.

Naye Dk Sarah Mwafalo,alisema ametembela Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa na kwamba amejifunza mambo mengi ya utalii na kwamba mbali na kutembelea maporomoko pia kitendo cha kutembea kwa miguu umbali wa  kilometa zaidi ya nne ni mazoezi muhimu kwa afya ya binadamu.

Sarah alisema kwamba wanawake wote waliotembelea Hifadhi hiyo mbali na kufanya utalii wa ndani pia wanafanya mazoezi na hivyo wameweza kuimarisha afya zao kwa ujumla hususani ya akili na pale watakaporudi kwenye majukumu yao watafanya kazi zao kwa ufasaha zaidi.

Kwa upande wake Elizabeth Tarimo mkazi wa Dodoma alisema kuwa ametumia usafiri wa Reli ya Mwendo kasi kutoka Dodoma kuja Morogoro kwa ajili ya kutalii Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa ambapo aliishukuru serikali kwa ujenzi wa reli hiyo na aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Morogoro ikiwemo Hifadhi ya Taifa Mikumi.

“Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia usafiri huu wa SGR hivyo natumia fursa hii kuwahamisisha wananchi wenzangu kutumia Reli ya Mwendo kasi kuja Morogoro kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio vilivyopo nchini hususani mkoa wa Morogoro.”

Naye Afisa Uhifadhi, Kitengo cha Utalii,Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa, Ahmed Nassoro alisema Hifidhi hiyo ni maarufu nchini kutokana na kuwa na viumbe adimu kama Mbega mwekundu wa Udzungwa,Ng’olaga wa Sanje,jamii za Ndege kama Chozi Mbawa Nyekundu na Kware wa Milima ya Udzungwa kuliko maeneo mengine yote na kwamba watalii wa ndani na nje wanaotembelea hifadhi hiyo huvutiwa na vivutio vyote vinavyopatikana hapo.

Ahmed Nassoro aliwataka Watanzania wote kuendelea kutembelea Hifadhi hiyo kwani kitendo cha kuona vivutio vinavyopatika katika Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa kutawafanya kuimarisha afya ya akili na pia kutawasaidia kujiepusha na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kwani ili ufike eneo husika mtu hulazimika kutembea kwa miguu kitendo kinachojenga mwili kwa mazoezi.

Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa maarufu kwakuwa na viumbe adimu duniani na maporomoko ya maji  hivyo  watalii wengi hutembelea Hifadhi ya Milima Udzugwa na kuchangia ongezeko la pato la Taifa.

Na. Zainabu Ally- Udzungwa

Chapisha Maoni

0 Maoni