WANANCHI wa
Kata ya Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wameishukuru Serikali
kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kurahisisha
mawasiliano ya barabara ya Malichewe na kuwapunguzia changamoto ya kutembea
umbali mrefu kutoka kata hiyo kwenda Sumbawanga Mjini.
Mhe. Andrea
Barnaba Diwani wa Kata ya Kizwite, ameishukuru serikali kwa kuwajengea barabara
hiyo kwani hapo awali kulikuwa na mashimo na makorongo makubwa ambapo magari na
bajaji yalikuwa yanapita kwa shida na kusababisha wananchi kupandishiwa nauli
kufika mjini.
“Tunaishukuru
serikali kwa kutuletea barabara ya lami, hapo awali wananchi walilazimika
kufanya mzunguko mkubwa na kutumia gharama kwenda mjini, walikuwa wanalipa
nauli shilingi 1000 lakini sasa hivi wanalipa shilingi 500 kufika mjini kufuata
huduma mbalimbali," alisema.
Naye, mkazi
wa Mtaa wa Mkumbuke, Bi. Veronica Mwanyeche amesema, zamani kipindi cha mvua
barabara hiyo ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa matope sasa hivi wanafika
mjini kwa urahisi na huduma nyingi zimewafikia huku wengine wakijenga nyumba za
kisasa kutokana na uwepo wa barabara nzuri.
Bw. Florence
January mkazi wa Kizwite Sokoni, anayejihusisha na kutoa huduma za kusafirisha
abiria amesema, hapo awali alikuwa anapata shida kusafirisha abiria kwa sababu
ya vumbi na matope hata hivyo baada ya matengenezo hayo hajapata changamoto
yoyote huku akiipongeza serikali kwa kuwajali wananchi wake.
Kwa upande
wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Sumbawanga, Mhandisi Dickson Kanyankole
amesema mradi wa barabara ya Malichewe yenye urefu wa Kilomita 1.2 umejengwa
kwa kiwango cha lami kwa thamani ya shilingi milioni 871 ambapo mradi
umekamilika na wananchi wanasafiri bila shida.
Ameongeza
kuwa kwa sasa wanajenga mita 800 na kipande kinachobakia mita 400 kitajengwa
mwaka wa fedha 2025/26 ili kukamilisha barabara nzima yenye Km 2.4 kwa kiwango
cha lami.
Hata hivyo,
ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya barabara
kwa kufanya usafi wa mitaro kwani ni wajibu wao kuitunza ili waendelee
kunifaika nayo kwa muda mrefu.

0 Maoni