Katika kuendelea kuifungua nchi
Kimataifa, Tanzania inaendelea kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika
Sekta ya Nishati kimataifa ikiwemo mpango wa kunadi vitalu vilivyo wazi nchini
kwa ajili ya utafutaji wa mafuta na Gesi Asilia.
Hayo yameelezwa leo Novemba 5, 2024 na
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio kwenye Kongamano la
Wiki ya Nishati 2024 (Africa Energy Week - AEW) ambalo linawakutanisha wadau wa
nishati ya mafuta, gesi asilia na nishati jadidifu kutoka barani Afrika na nchi
nyingine duniani jijini Cape Town nchini Afrika Kusini.
"Tanzania inatumia kongamano hili
kueleza fursa nyingine za uwekezaji katika vitalu vya utafutaji wa mafuta na
gesi asilia alivyopewa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja
na fursa zilizopo katika mkondo wa kati na wa chini wa petroli ikiwemo miradi
ya Mini LNG," amesena Dkt. Mataragio.
Ameongeza kuwa, Mamlaka ya Mkondo wa
Juu wa Petroli (PURA) itakuwa na banda la maonesho kwa kushirikiana na TGS
ambapo masuala mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli yataoneshwa pamoja na
maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia
vilivyo wazi nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mataragio
ameeleza kuwa, kongamano la AEW litavutia washiriki wengi duniani kwakuwa
limekidhi mwelekeo wa dunia wa kuondokana na nishati chafuzi za mazingira.
Dkt. Mataragio ameongeza kuwa,
washiriki kutoka Tanzania wataweza kukutana na kampuni mbalimbali za mafuta na
gesi asilia duniani ikiwemo Schlumber Company Ltd.
Kwa mwaka 2024, kongamano hilo ni la
30 na linafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 8 novemba nchini humo na kuhusisha
wadau wa nishati zote duniani.
0 Maoni