Mradi wa
Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na
Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), leo tarehe 11, Novemba 2024
umekabidhi magari madogo sita (6) ya kwa ajili ya hifadhi za Nyerere, Ruaha,
Mikumi na Udzungwa, Hifadhi ambazo ziko ndani ya mradi huo unaotekelezwa kusini
mwa Tanzania.
Akipokea
magari hayo Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji aliishukuru Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuhakikisha kuwa uhifadhi unapata kipaumbele kupitia miradi mbalimbali kwa
faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
“Kupitia
mradi huu, hadi sasa tumefanikiwa kupata jumla ya magari madogo 41 yakiwemo
magari haya yanayokabidhiwa siku ya leo. Ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono ya kuhakikisha kuwa
uhifadhi unapata kipaumbele kupitia miradi mbalimbali na nitoe wito kwa hifadhi
zinazofaidika na magari haya kuyatunza, na kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa,”alisema
Kamishna Kuji.
Aidha,
Kamishna Kuji aliipongeza Benki ya Dunia kwa msaada wao katika kufanikisha
mradi huu na kubainisha kuwa mchango wao si tu unasaidia juhudi za uhifadhi,
bali pia unakuza uchumi wa jamii kupitia fursa za ajira na uwezeshaji wa jamii
zinazozunguka hifadhi za Taifa.
Naye, Kamishna
Msaidizi wa Uhifadhi, Maureen Mwaimale ambaye ni mhasibu wa mradi wa REGROW
alibainisha kuwa mradi huo umekabidhi magari madogo sita (6) ya nyongeza kwa
ajili ya hifadhi za Nyerere, Ruaha, Mikumi na Udzungwa ikiwa ni ufadhili wa
kupitia mkopo wa masharti nafuu uliotolewa na Benki ya Dunia kwa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuongeza kuwa magari hayo yana thamani ya
jumla ya Shilingi za Kitanzania takribani milioni mia nane na ishirini na
yatatumika kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa athari za mazingira baada ya
ukamilishwaji wa shughuli za ujenzi ndani ya hifadhi pamoja na kuwezesha jamii
na kuhakikisha usalama wa jamii na mazingira (safe guard).
“Hifadhi
zilizopo chini ya mradi wa REGROW zimekwishapokea vifaa vya doria, vifaa vya
TEHAMA, mitambo ya barabara 16, malori makubwa 44 yakiwepo magari ya kutoa
elimu ya uhifadhi (Cinema Vans and Epxedition Vehicles), matrekta saba, magari
41 yakiwemo haya sita,” alisema Kamishna Mwaimale.



0 Maoni