Kamishna wa
Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji amesisitiza ushirikiano ili kusukuma mbele
jukumu la maendeleo ya Shirika na kutimiza malengo yaliyowekwa kwa wakati.
Kamishna
Kuji, ameyasema hayo katika ziara yake aliyoifanya jana katika Hifadhi ya Taifa
Tarangire ikiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na
utalii pamoja na kuzungumza na Maafisa na Askari uhifadhi waliopo katika
hifadhi hiyo.
“Tushirikiane
kwa pamoja ili kusukuma mbele jukumu la maendeleo ya Shirika letu na nisisitize
kufanya kazi kwa pamoja kama timu moja ili tutimize malengo ya Shirika kwa
wakati.”
“Tunapoona
tunapata tuzo mbalimbali na kutambuliwa kimataifa ni kutokana na ushirikiano
katika kazi na mchango wa kila mmoja
wetu, hivyo nasisitiza yule mkubwa kwa cheo na mdogo kuheshimiana na
kuthaminiana ili kuleta tija katika utendaji kazi,” alisema Kamishna Kuji.
Aidha,
Kamishna Kuji aliipongeza Hifadhi ya Taifa Tarangire kwa kuendeleza juhudi za
kuhifadhi na kutangaza vivutio vilivyopo ili kuvutia wageni wengi zaidi
kutembelea hifadhi hiyo ambayo ni hifadhi ya tatu kwa mapato katika Shirika.
Awali,
akiwasilisha taarifa ya hifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi,
Beatrice Kessy ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire alibainisha kuwa hifadhi
hiyo kwa kipindi cha miezi minne ya mwaka huu wa fedha imeweza kukusanya kiasi
cha shillingi Billioni 32 na kuongeza kuwa hifadhi hiyo imeandaa mkakati
kabambe utakao kwenda kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato na kufikia kiasi
cha shillingi billioni 100 ifikapo mwaka 2030.
Hifadhi ya
Taifa Tarangire ni miongoni mwa hifadhi zilizopo katika Kanda ya Kaskazini na
ni maarufu kwa makundi makubwa ya tembo wanaoonekana kwa urahisi na kuwa
kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.



0 Maoni