WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana
na Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Shirikisho la Urusi, Bw. Maxim Reshetnikov
na kujadiliana naye masuala mbalimbali yakiwemo yanayogusa biashara, kilimo,
usafirishaji, elimu, nishati na utalii.
Akizungumza na Waziri Reshetnikov leo
(Jumatatu, Oktoba 28, 2024) ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu amemhakikishia Waziri huyo kwamba Tanzania ni mahali pazuri pa
kufanya biashara kwa kuwa ni nchi tulivu na Mwenyezi Mungu ameiweka mahali pa
kimkakati pa kuweza kufanya biashara.
“Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia
Suluhu Hassan imejipambanua kufanya maboresho kwenye biashara kati ya Tanzania
na nchi marafiki, Urusi ikiwemo. Kupitia ziara hii, nina uhakika mtapata
maelezo mazuri ambayo yatawatia moyo wa kuiamini Tanzania kwamba ni mahali
pazuri pa kufanyia biashara,” amesema.
Akielezea kuhusu fursa zilizopo
nchini, Waziri Mkuu amesema Tanzania inapakana na bahari yenye bandari za Dar
es Salaam, Mtwara na Tanga. “Ina maziwa ya Victoria, Tanganyika, Nyasa na yenye
bandari kadhaa. Ziwa Victoria kuna bandari kule Kagera, Mwanza na Musoma. Ziwa
Tanganyika kuna bandari za Kigoma, Kabwe na Kasanga na Ziwa Nyasa kuna bandari
za Mbambabay na Kyela.”
Amesema bandari hizo zimeunganishwa na
barabara, reli ya kati, TAZARA, reli ya SGR na vyote vinaenda hadi nje ya nchi
ili kurahisihwa usafirishaji wa bidhaa. “Tunao usafiri wa uhakika kutoka Dar es
Salaam hadi Kapiri-Mposhi, Zambia ambako bidhaa zinachukuliwa na kupelekwa nchi
nyingine. Pia SGR itakapokamilika, itawezesha kufikisha mizigo hadi Rwanda,
Uganda na Congo.”
Kuhusu kilimo, Waziri Mkuu
amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Urusi waje kuwekeza kwenye kilimo kwa
kuwa Tanzania ina eneo kubwa la ardhi na lenye rutuba kwa ajili ya shughuli za
uzalishaji. “Malengo ya Tanzania ni kuona tunakuwa kitovu cha uzalishaji wa
chakula barani Afrika.”
Ametumia fursa hiyo kumweleza faida
mbalimbali za kuwekeza Tanzania kubwa ikiwa ni uhakika wa wateja kwa bidhaa zao
kwani yenyewe ina wakazi zaidi ya milioni 61, ukanda wa Afrika Mashariki una
watu zaidi ya milioni 300 na pia nchi za SADC ambako Tanzania ni wanachama, una
uhakika wa soko la watu zaidi ya milioni 300.
“Tanzania ni lango kwa nchi nane
zinazotuzunguka na mbili ziko mbioni kujiunga. Nchi hizo ni Kenya, Uganda, DRC,
Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji. Kuna nchi mbili za Comoro na Sudan
Kusini ambazo nazo zimeonesha nia na pia Somalia tunaendelea na mazungumzo.”
Mapema, akitoa maelezo ya ujio wake,
Waziri Reshetnikov alisema nchi hizo mbili zimeshakubaliana kuimarisha
ushirikiano wa kiuchumi, kukuza biashara na uwekezaji na ndiyo maana kesho
(Jumanne, Oktoba 29, 2024) watakuwa na kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya
Kiserikali ya Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Tanzania na Urusi chenye nia ya
kuimarisha uhusiano huo.
Alisema kikao hicho ni matokeo ya
makubaliano ya kuanzishwa kwa Tume hiyo ya pamoja ambayo yalisainiwa Desemba
29, 2022 ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi.
Kwa upande wa elimu, Waziri huyo
alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Watanzania kunufaika na fursa za masomo
nchini Urusi kutokana na bajeti ya Serikali. “Hivi sasa kuna nafasi 90 za
wanafunzi wa Kitanzania kusomea vyuo vikuu vya Urusi kuanzia mwaka ujao. Tuko
tayari kuongeza idadi hiyo endapo itabidi,” alisema Waziri Reshetnikov.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akizungumza na Waziri wa Uchumi na
Maendeleo wa Shirikisho la Urusi Maxim Reshtnkov na ujumbe wake, katika Ofisi
Ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam, Oktoba 28, 2024. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipeana
mkono na Waziri wa Uchumi na Maendeleo
wa Shirikisho la Urusi Maxim Reshtnkov, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu
Magogoni jijini Dar es Salaam, Oktoba 28, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
0 Maoni