Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka
Wizara ya Nishati kuendelea kuusimamia ipasavyo Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa
Julius Nyerere (JNHPP) ili ukamilike kwa wakati.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.
Kirumbe Ng'enda jana wakati wa ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi
huo ambao utaingiza megawati 2,115 mara baada ya kukamilika.
"Wizara iendelee kusimamia kwa umakini mradi huu ili
mashine zote Tisa ziweze kukamilika kama ilivyopangwa," amesema Mhe.
Ng'enda.
Aidha, kamati hiyo imeipongeza Serikali kwa kuhakikisha
mashine zilizosalia zinaendelea kukamilika na kufanya kazi ambapo hadi sasa
zimekamilika mashine tatu ambazo zinazalisha kiasi cha megawati 705 na mashine
namba sita ipo kwenye hatua za mwisho kukamilishwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga
amesema Wizara ya Nishati imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na kamati hiyo
ya Bunge ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo, ushauri na mapendekezo ya
Kamati.
"Kazi kubwa ya Kamati ni kutusimamia sisi Serikali, na
sisi tunahakikisha kuwa maelekezo yenu yote yanatekelezwa na mafanikio yake
yanaonekana katika miradi mbalimbali kama JNHPP ambao utekelezaji wa mradi wake
umefikia asilimia 98," amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati chini ya Naibu Waziri Mkuu
na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko itaendelea kuusimamia mradi huo ila
ukamilike kwa wakati.
Ameeleza kuwa, Mkandarasi wa mradi ameshalipwa takriba shilingi trilioni 6.3 kati ya shilingi trillioni 6.5 zinazopaswa kulipwa.

0 Maoni