Serikali yajizatiti kutumia mbinu za kisayansi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu

 

Katika kuhakikisha inakabiliana kikamilifu na changamoto ya Wanyama wakali na waharibifu hapa nchini, Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka wa fedha 2024/2025 imejipanga kugharamia matumizi ya mbinu mchanganyiko za Kisayansi.

Mbinu hizo za kisayanzi zinajumuisha matumizi ya Mabomu baridi yaliyoboreshwa na kuzalishwa hapa nchini kufuatia utafiti wa kisayansi uliofanywa kwa ushirikiano kati ya TAWIRI na Jeshi la Wananchi wa Tanzania - Mzinga, matumizi ya mikanda ya mawasiliano na visukuma mawimbi, matumizi ya ndege Nyuki (Drones); pamoja na matumizi Helkopta kwa ajili ya kufukuzia tembo kwenye maeneo yenye changamoto.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) kwa nyakati tofauti  katika vijiji vya Milola kilichopo jimbo la Mchinga na kijiji cha Chidyoya kilichopo Jimbo la Mtama akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Lindi kuwaeleza wananchi juu ya jitihada zinazofanywa na Serikali kudhibiti changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.

Aidha, aliongeza kuwa serikali imepanga kugawa mabomu baridi yapatayo 1000 kwa majimbo hayo mawili ili yatumike kufukuzia wanyama wakali na waharibifu.

Mhe. Kitandula aliendelea kusema kuwa serikali inafahamu changamoto za wanyama wakali na waharibifu, na ndio maana inaweka juhudi kubwa za kutatua changamoto hiyo.

“Mwaka wa fedha unaokuja wizara ya maliasili na utalii ikishirikiana na wadau wa maendeleo imepanga kusomesha VGS wengi zaidi na kuwapatia vitendea kazi vya kutosha ili kuweza kuwa na askari wengi zaidi katika maeneo ya vijiji ambao watafanya kazi kwa kushirikiana na askari wetu wa jeshi la uhifadhi kuhakikisha wananchi hawaendelei kupata kadhia ya wanyama wakali na waharibifu.”

Mhe. Kitandula alisema kuwa kwa sasa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori  (TAWIRI) ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasil na Utalii inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuboresha mbinu zilizopo, na halikadhalika kuibua mbinu bora zaidi zitakazosaidia kupambana na wanyama wakali na waharibifu.

Mhe. Kitandula alihitimisha hotuba kwa kutoa Rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutokuchelewesha taarifa za tathimini ya majanga yanayosababishwa na wanyama wakali na waharibifu; na amewataka kutumia sehemu ya fedha za mapato ya ndani yatokanayo na vyanzo vya maliasili zinazopatikana katika maeneo yao kuwezesha mchakato wa upatikanaji wa tathmini hizo kutoka ngazi ya halmashauri.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Lindi Mhe. Zainabu Telak wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii amelishukuru sana jeshi la uhifadhi linalojumuisha Taasisi ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), TANAPA na TFS kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kupambana na wanyama wakali na waharibifu hususan Tembo.

“Mhe. Naibu Waziri nalipongeza sana jeshi la uhifadhi kwani wamekuwa wakitoa ushirikiano wa dhati pale ambapo kumekuwa na tatizo la wanyama wakali na waharibifu lakini changamoto kubwa tuliyonayo ni uchache wa askari na vitendea kazi, naomba muone jinsi ambavyo mtaweza kutuongezea askari na vitendea kazi. Shukrani zangu hizi pia naomba umfikishie Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Angellah Kairuki kwani wote kwa pamoja mmekuwa msaada mkubwa pale ambapo kumekuwa na tatizo la wanyama wakali na waharibifu,” alisema Mhe. Telak. 


Na Anangisye Mwateba-Lindi

Chapisha Maoni

0 Maoni