Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Philip Isdori Mpango ameielekeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
na ile ya Ulinzi kwenda eneo la Oldonyosambu lilipo wilaya ya Arumeru mkoa wa
Arusha kusikiliza na kutafuta suluhu ya changamoto ya wananchi na shamba la
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Dkt. Mpango ametoa maelekezo jana akiwa katika eneo la Oldonyosambu
aliposimamishwa na wananchi barabarani wakitaka kusikikizwa changamoto
zinazowakabili wananchi wa eneo hilo
ikiwemo ya maji, barabara, umeme na shamba la Jeshi la Kujenga Taifa.
Katika kutoa majibu ya mgogoro huo. Dkt. Mpango aliwaambia
wananchi hao kuwa, anawaelekeza mawaziri wa wizara hizo mbili kwenda eneo
husika kwa lengo la kukutana na kuwasikiliza wananchi wa eneo hilo ili kutafuta
suluhu ya mgogoro huo.
"Naibu Waziri wa Ardhi, nakutaka urudi hapa ukiwa na
mwenzako waziri wa ulinzi ulimalize jambo hili," alisema Mhe Dkt. Mpango.
Awali wakati wa mkutano wa hadhara mara baada ya Makamu wa
Rais Mhe Dkt Mpango kuzindua miradi ya umeme na kituo cha Afya Ketumbeine,
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda
aliwaeleza wananchi wa Longido kuwa, wilaya hiyo kwa sasa iko shwari kwa kuwa changomoto pekee iliyopo
katika eneo la ardhi ni ile ya mipaka ya wilaya aliyoieleza kuwa inafanyiwa
kazi.
"Migongano hapa Longido imetulia na changamoto iliyopo
ni ya mipaka ya wilaya na zipo timu zinafanyia kazi, niwashukuru wakuu wa
wilaya kwa kazi kubwa ya kuwapa utulivu wananchi," alisema Mhe. Pinda.
Aidha, Mhe. Pinda ameonya wale wote wanaovamia maeneo ya ardhi na kuahidi wizara yake kushirikiana na wakuu wa wilaya katika kudhibiti uvamizi huo huku akitoa wito kwa watanzania kuwa, ardhi haiongezeki pamoja na idadi ya watu kuongezeka na kutaka busara kutumika katika kuitumia ardhi.
Na. Munir Shemweta- WANMM Arusha
0 Maoni