Mfanyabiashara aitoa nyumba yake iwe Kituo cha Polisi

 

Mfanyabiashara na Mkazi wa Kata ya Ilangala, kisiwa cha Gana, Nyamichere Ogunya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza amejitolea nyumba yake aliyokuwa anaitumia na kuikabidhi kwa Jeshi la Polisi ili iwe Kituo cha Polisi kwa ajili ya kutoa huduma za Usalama kwa wakazi zaidi ya 6,000 wa kisiwa hicho.

Nyumba hiyo yenye vyumba zaidi ya 15 imekabidhiwa kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza (SACP) Wilbroad Mutafungwa ambapo amemshukuru mfanyabiashara huyo, na kusema baada ya nyumba hiyo kufanyiwa marekebisho kwa kuwekewa miundombinu na mifumo ya majitaka itakayokidhi hadhi ya Kituo cha Polisi itaanza kutumika kutoa huduma kwa wakazi wa kisiwa hicho.

"Nimpongeze mfanyabiashara aliyejitolea nyumba yake kuwa kituo cha polisi na ikiwezekana marekebisho ya kituo hiki natamani yaishe mwishoni mwaka mwaka huu ili mwezi Januari 2024 pengine kituo hicho kiwe kimekamilika na mimi nitatamani sana kuja kukizindua hiki kituo ili tuweke askari wa kutosha kuanza kufanya kazi," amesema Kamanda Mutafungwa.

Swai Somba ni mvuvi wa kisiwa hicho ameliomba Jeshi la Polisi kusaidia kukamilisha mapema marekebisho ya kituo hicho ili huduma ianze kutolewa itakayosaidia kukomesha vitendo vya uhalifu huku akiomba mipaka inayotenganisha Tanzania na Uganda iwekwe ziwani ili kupunguza matukio ya wavuvi wa pande hizo mbili kuingiliana.

"Sisi wavuvi wadogo tunapotoka hapa kisiwani kuingia ziwani huko kuvua huwa tunanyanyasika sana kutokana na vyombo vyetu mfano sisi wavuvi wa kasia huwa uvuvi wetu ni duni lakini wanaotumia mashine wametuwekea masharti ambayo mimi ninashindwa kujua moja wapo ukitoka ziwani ukileta hapa samaki unaanza kuulizwa umetumia zana gani kuvua wakati huenda ulikuwa na ndoano, tunaomba msaada katika hili," amesema Somba.

Mwenyekiti wa Kamati ya ushauri na uvuvi endelevu Ziwa Victoria, Bakari Kadabi amesema, kuanzia Januari 2024, Serikali inatarajia kuweka mipaka ziwani itakayokuwa inawasaidia wavuvi kujua upande wa Tanzania na Uganda.

"Kuhusu mipaka Serikali imejipanga kuanzia mwezi Januari kuweka maboya mpakani kati ya Tanzania na nchi jirani kwa hiyo tatizo la kuingilia linaenda kuisha kabisa ila niwaombe wavuvi muwe wakweli hamna sababu ya kwenda kuvua upande wa Uganda wakati huku tuna maeneo mengi ya kuvua," amesisitiza Kadabi.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa ametangaza kufanya oparesheni kabambe na endelevu ndani ya Ziwa Victoria na maeneo mengine ili kutokomeza uhalifu na kuimarisha ulinzi na usalama zaidi katika maeneo yote.

Chapisha Maoni

0 Maoni