Mbunge wa Segerema CCM, Mhe. Tabasamu Hamisi, ameishauri
Serikali kuondoa kamari na vipodozi kuwa vyanzo vya mapato vya Mfuko wa Bima ya
Afya kwa Wote na badala yake itafute vyanzo vingine vya mapato.
Akichangia bungeni Dodoma leo hoja ya Muswada wa kuanzishwa
kwa Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote Mhe. Tabasamu ameishauri Wizara ya Fedha na
Mipango kutafuta vyanzo vingine vya mapato ya kuchangia mpango huo.
“Mimi nashauri vyazo vya mapato ya bima hii visiwe vya
michezo ya kamari, hivi mtu mcha Mungu kama mimi leo hii naugua natibiwa na
fedha za kamari, hii itakuwaje,” alihoji Mhe. Tabasamu na kuongeza, “Na vipodozi
pia nafikiri ni vyema kuondolewa kama vyanzo vya mapato ya bima hii, yaani tunataka
wanawake waache kujipodoa wafanane na sisi wanaume haiwezekani”.
Aidha, Mhe. Tabasamu alionyesha kushangazwa na tukio la
mmoja wa diwani wa jimbo lake aliyekuwa na bima aliyefariki akipatiwa matibabu
hospitalini, na kisha kudaiwa gharama za mochwari kwa madai kuwa bima yake
imekufa baada tu ya kufariki dunia.
“Mheshimiwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu naomba utakapokuja
kukamilisha hoja yako utoe majibu inawezekanaje mtu akifa tu na bima yake
inakufa, mimi nadhani bima inatakiwa kuendelea na kukoma pale mtu atakapozikwa,”
alisema Mhe. Tabasamu.
Kwa upande wake Mbunge wa Bushosha CCM, Mhe. Eric Shigogo,
akichangia hoja hiyo aliishauri Serikali kutilia mkazo katika kuhakikisha
mifumo ya vipimo ya hospitali inasomana ili kuondoa mzigo kwa NHIF wa gharama
za vipimo kila mgonjwa anapopewa rufaa kwenda hospitali nyingine.
“Sasa hivi mgonjwa akipimwa vipimo Muhimbili, akaenda MOI
inabidi vipimo vyote alivyopima Muhimbili aanze kupima upya MOI jambo ambalo
linaiongezea gharama mfuko huu na linaweza kuchangia kuua mfuko,” alisema Mhe.
Shigongo.
Mhe. Shigongo pamoja na kuunga mkono hoja pia, alishauri
kuboreshwa mfumo wa kudhibiti udanganyifu kwani kwa sasa kadi ya bima ya NHIF
inatumika vibaya na baadhi ya watu kwa kushirikiana na madaktari wa baadhi ya hospitali
za binafsi na kuiibia Serikali.
“Watu sasa wanatumia vibaya bima, mtu anakwenda hospitali
anamuambia Daktari ninashida ya shilingi 30,000 anampatia kadi Daktari, Daktari
anafanya anachotaka na kadi hiyo na mwisho wa siku mzigo unarudi kwa NHIF,”
alisema Mhe. Shigongo.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Shigongo ameshauri Mfuko wa Bima
ya Afya kwa wote utenge sehemu ya fedha japo asilimi mbili kwa ajili ya kuhamasisha
kinga kwa jamii, kwa kutoa elimu ya lishe bora na kujenga maeneo ya kufanyia
mazoezi ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
0 Maoni