Moto umeunguza majengo kadhaa, maduka, vibanda na migahawa
katika eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam, na kuwaacha wafanyabiashara
wakiangua vilio, hali iliyobua taharuki kwa muda katika eneo hilo ambalo ni
kitovu cha biashara.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alifika
katika eneo hilo la moto na kuwaeleza waandishi wa habari kwamba moto huo
ulianza katika jengo moja na baadae majengo machache yakashika moto.
Amesema kuwa hadi majira ya saa nne asubuhi hakukuwa na
taarifa yoyote ya mtu aliyepoteza maisha katika tukio hilo la moto, lakini kuna
baadhi ya watu watapata hasara za mali na majengo yaliyoungua moto.
Ameongeza kuwa wamebaini kati ya jengo na jengo vichochoro
vimezibwa, na uongozi ulishaagiza vichochoro hivyo vizibuliwe ili kuwezesha kupatikana
namna ya kupita pindi panapotokea janga la moto ili kuwe na namna ya kuzima.
"Nyinyi wenyewe (waandishi wa habari) mmeona vichochoro
vimezibwa na mabanda, na mabanda yenyewe yamejengwa kwa mbao jambo ambalo
limesaidia kuchochea kuwaka zaidi kwa moto uliotokea," alisema RC
Chalamila.
Chalamila amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kulinda mali na raia, pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, “Wamejitahidi
sana, mpaka muda huu zimamoto wamekata moto usiendelee kwenye majengo mengine
na kuendelea kuzima majengo yaliyoungua.”
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo moto huo ulianza majira
ya saa 12 alfajiri, ambapo majirani walihaha kuwapigia simu wahusika ili kuwahi
kuokoa bidhaa zao ambapo baadhi yao walifanikiwa kuokoa bidhaa na wengine
walishindwa baada ya moto kushika kasi.
Jeshi la Polisi lilionekana likiwa limeimarisha ulinzo
katika eneo hilo lililotokea moto ili kudhibiti wahalifu wasifanye vitendo vya
kupora bidhaa katika maduka hayo, wakisaidiana na wananchi waliokuwapo.
Kufuatia moto huo barabara ya Mtaa wa Msimbazi ilifungwa kwa
muda kwa zaidi ya saa tatu baada ya kutokea moto huo, ambapo watumiaji wa
barabara hiyo walilazimika kutumia barabara mbadala kwa muda.
0 Maoni