Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Philip Mpango ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza katika utoaji wa elimu
bora na kutoa huduma bora za afya kwa wananchi ili kuwa na rasilimali watu
wenye nguvu watakaoweza kuzalisha kwa tija.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati
akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kufungua Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mtaji
Rasilimali Watu unaofanyika kuanzia Julai 25-26, 2023 katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa (JNICC).
Mhe. Dkt. Mpango amesema inakadiriwa kuwa, katika nchi za
kipato cha chini na cha kati, karibu asilimia 40 ya watu wenye umri wa miaka 0
hadi 14 wanaohudhuria shule watakuwa wanatoka Afrika ifikapo mwaka 2050. Aidha,
umaskini wa kujifunza utaongezeka kwa asilimia 10 hadi zaidi ya asilimia 60
katika nchi zinazoendelea duniani kote na kutoka asilimia 83 hadi zaidi ya
asilimia 90 katika nchi masikini.
"Kutokana na takwimu hizo, Afrika inahitaji kuchukua
hatua za haraka kushughulikia idadi ya watu kwa kufanya uwekezaji mzuri katika
afya ya watu wetu na elimu ya hali ya juu ambayo itawapa vijana wetu ujuzi
unaohitajika kwa mafanikio ya kiuchumi ya nchi zetu", amebainisha Dkt.
Mpango.
Aidha, ameongeza kuwa, Kauli mbiu ya Mkutano huo ya
"Kuharakisha Ukuaji wa Uchumi wa Afrika: Kuongeza Uzalishaji wa Vijana kwa
Kuboresha Kujifunza, Ujuzi na Uzalishaji wa Vijana" inakumbusha uwezo wa
vijana kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi mbalimbali ikiwa nchi
zitawekeza kwa uangalifu katika elimu, ujuzi na matarajio ya vijana hao.
"Ni matarajio yangu kwamba Mkutano huu utajitahidi
kupanga malengo kufikia ajenda hiyo ya rasilimali watu na wito wangu kwetu sote
pamoja na Washirika wetu wa Maendeleo ni kuhamasisha rasilimali kwa ajili ya
uwekezaji katika kujifunza, afya, lishe, maendeleo jumuishi na ulinzi wa
kijamii", amefafanua Dkt. Mpango.
Kutokana na hayo Dkt. Mpango ametoa rai kwa wataalam wote
waliohudhuria mkutano huo, kuja na sera za ubunifu ambazo zitaboresha matokeo
ya mtaji wa rasilimali watu kwa Afrika kwa kuzingatia idadi kubwa ya vijana,
pia ameshauri Taasisi za Fedha za kikanda kujitahidi kupata ufumbuzi wa
changamoto za kifedha ili kuunga mkono msukumo wa Afrika wa kuharakisha
maendeleo ya mtaji wa rasilimali watu.
Vilevile, ameshauri mkutano huo kujadili jinsi sekta binafsi
inavyoweza kuhamasishwa kushirikiana kikamilifu na serikali kama wadhamini na
wazalishaji wa mtaji bora wa rasilimali watu, pia taasisi za mafunzo za
kiafrika ambazo ni nguzo muhimu katika uendelezaji mtaji wa rasilimali watu
zinaweza na zinapaswa kusaidia Bara la Afrika kuimarisha uwezo wa ndani
kusimamia na kutumia vyema rasilimali zilizopo.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

0 Maoni